Kuhusu injili ya Marko

Injili ya Marko ni rekodi ya kale iliyoandikwa zaidi ya Yesu wa Nazareti, iliyoandikwa karibu 65 BK na rafiki wa karibu wa Yesu na mwanafunzi wake, Petro. Marko ni sehemu ya Biblia Takatifu - kitabu cha pili cha Agano Jipya. Sura zake 16 zilizojaa vitendo vinafunua utambulisho wa kipekee, mafundisho na kazi ya Yesu. Injili inamaanisha 'habari njeri', na Marko anaelezea kitabu hiki kama “habari njema juu ya Yesu Masihi”.

Injili ni nini?

Biblia Takatifu inatufundisha kwamba watu wote wanastahili aibu na hukumu kwa dhambi zetu. Lakini habari njema ni kwamba Yesu alikufa msalabani na kuchukua hukumu tunayostahili. Alifufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu ili kuthibitisha kwamba amelipa dhambi ya kila mtu anayemwamini. Na tunapotumaini Yesu kama Bwana na Mwokozi, Mungu anatusamehe kikamilifu na milele. Tunapata uhusiano halisi na uliorejeshwa na Mungu ambao hautaishia kamwe.

Vidokezo vya kusoma

Unaweza kuvinjari kitabu hiki kwa nambari za sura na aya (angalia viungo chini ya ukurasa ili kubadilisha sura). Kwa mfano, 'Marko 8:29' inahusu Marko sura ya 8, aya ya 29. Kwa sababu Biblia ni kitabu cha zamani kutoka mahali pengine, kuna mambo mengi ambayo unaweza kuwa vigumu kuelewa mwanzoni. Hii inapotokea, ombe msaada wa Mungu, na fikiria kusoma kitabu na mfuasi mwenye uzoefu wa Yesu. Maoni ya mtandaoni kama vile bibleref.com pia yanaweza kukusaidia unapojifunza.

Marko

Marko 1

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
1 Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, 2kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:
“Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,
atakayetengeneza njia mbele yako”:
3 “sauti ya mtu aliaye nyikani,
‘Itengenezeni njia ya Bwana,
yanyoosheni mapito yake.’”
4 Yohana Mbatizaji alikuja akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5Watu kutoka Yudea yote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. 6Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Alikula nzige na asali ya mwitu. 7Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. 8Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”
9 Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani. 10Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua. 11Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”
12 Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu hadi nyikani, 13naye Yesu akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama pori, nao malaika wakamhudumia.
14 Baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu alienda Galilaya, akaanza kuhubiri Habari Njema ya Mungu, 15akisema, “Wakati umetimia, ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”
16 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa walikuwa wavuvi. 17Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 18Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.
19 Alipoenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.
21 Wakaenda hadi Kapernaumu. Mara ilipofika siku ya Sabato, Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha. 22Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. 23Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye akapaza sauti akisema, 24“Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”
25 Lakini Yesu akamkemea, akamwamuru, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” 26Yule pepo mchafu akamgaragaza huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.
27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” 28Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.
29 Mara walipotoka katika sinagogi, walienda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani mwa Simoni na Andrea. 30Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. 31Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.
32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.
35 Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba. 36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta, 37nao walipomwona, wakapaza sauti, wakasema, “Kila mtu anakutafuta!”
38 Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine, kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia. Maana nilikuja kwa kusudi hili.” 39Kwa hiyo akazunguka Galilaya yote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.
40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akapiga magoti, akimwomba, “Ukitaka, unaweza kunitakasa.”
41Yesu, akiwa amejawa na huruma, akaunyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” 42Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika.
43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake mara moja; 44akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” 45Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi bali alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

Unataka kwenda wapi baadaye?