Kuhusu injili ya Marko

Injili ya Marko ni rekodi ya kale iliyoandikwa zaidi ya Yesu wa Nazareti, iliyoandikwa karibu 65 BK na rafiki wa karibu wa Yesu na mwanafunzi wake, Petro. Marko ni sehemu ya Biblia Takatifu - kitabu cha pili cha Agano Jipya. Sura zake 16 zilizojaa vitendo vinafunua utambulisho wa kipekee, mafundisho na kazi ya Yesu. Injili inamaanisha 'habari njeri', na Marko anaelezea kitabu hiki kama “habari njema juu ya Yesu Masihi”.

Injili ni nini?

Biblia Takatifu inatufundisha kwamba watu wote wanastahili aibu na hukumu kwa dhambi zetu. Lakini habari njema ni kwamba Yesu alikufa msalabani na kuchukua hukumu tunayostahili. Alifufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu ili kuthibitisha kwamba amelipa dhambi ya kila mtu anayemwamini. Na tunapotumaini Yesu kama Bwana na Mwokozi, Mungu anatusamehe kikamilifu na milele. Tunapata uhusiano halisi na uliorejeshwa na Mungu ambao hautaishia kamwe.

Vidokezo vya kusoma

Unaweza kuvinjari kitabu hiki kwa nambari za sura na aya (angalia viungo chini ya ukurasa ili kubadilisha sura). Kwa mfano, 'Marko 8:29' inahusu Marko sura ya 8, aya ya 29. Kwa sababu Biblia ni kitabu cha zamani kutoka mahali pengine, kuna mambo mengi ambayo unaweza kuwa vigumu kuelewa mwanzoni. Hii inapotokea, ombe msaada wa Mungu, na fikiria kusoma kitabu na mfuasi mwenye uzoefu wa Yesu. Maoni ya mtandaoni kama vile bibleref.com pia yanaweza kukusaidia unapojifunza.

Marko

Marko 10

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
1 Yesu akaondoka huko, akavuka Mto Yordani, akaenda sehemu za Yudea. Umati mkubwa wa watu wakaenda kwake tena, naye akawafundisha, kama ilivyokuwa desturi yake.
2 Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?”
3Yesu akawajibu, “Je, Musa aliwaamuru nini?”
4 Wakajibu, “Musa aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”
5 Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 6Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke’. 7‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, 8na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. 9Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
10Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili. 11Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye. 12Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”
13 Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea. 14Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 15Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.” 16Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
17 Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
18Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 19Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’”
20Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
21 Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!”
24 Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika ufalme wa Mungu. 25Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
26Wanafunzi wake wakashangaa sana. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
27 Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha kila kitu na kukufuata wewe!”
29Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au mama au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, 30ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu: nyumba, ndugu wa kiume na wa kike, mama na baba na watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao. 31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”
32 Walikuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa amewatangulia. Wanafunzi wake walishangaa, nao watu waliowafuata walijawa na hofu. Yesu akawachukua tena wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia yatakayompata. 33Akasema, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atasalitiwa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Wao watamhukumu kifo na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa, 34ambao watamdhihaki na kumtemea mate, watampiga na kumuua. Siku tatu baadaye atafufuka.”
35 Kisha Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakaja kwake na kumwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie lolote tutakalokuomba.”
36Naye akawaambia, “Je, mwataka niwafanyie jambo gani?”
37 Wakamwambia, “Tupe kukaa mmoja upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”
38 Lakini Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?”
39 Wakajibu, “Tunaweza.”
Kisha Yesu akawaambia, “Kikombe nikinyweacho mtakinywea na ubatizo nibatizwao mtabatizwa, 40lakini kuketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto si juu yangu mimi kuwapa. Nafasi hizi ni kwa ajili ya wale walioandaliwa.”
41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. 42Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao. 43Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 44na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote. 45Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
46 Kisha wakafika Yeriko. Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mmoja, jina lake Bartimayo (maana yake “mwana wa Timayo”), alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada. 47Aliposikia kuwa ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita, akaanza kupaza sauti akisema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
48Watu wengi wakamkemea, wakamwambia akae kimya, lakini yeye akazidi kupaza sauti, akisema, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
49Yesu akasimama na kusema, “Mwiteni.”
Hivyo wakamwita yule mtu kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Inuka, anakuita.” 50Akiwa analivua lile joho lake, alisimama na kumwendea Yesu.
51 Yesu akamuuliza, “Unataka nikufanyie nini?”
Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona.”
52Yesu akamwambia, “Nenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona, akamfuata Yesu njiani.

Unataka kwenda wapi baadaye?