Kuhusu injili ya Marko

Injili ya Marko ni rekodi ya kale iliyoandikwa zaidi ya Yesu wa Nazareti, iliyoandikwa karibu 65 BK na rafiki wa karibu wa Yesu na mwanafunzi wake, Petro. Marko ni sehemu ya Biblia Takatifu - kitabu cha pili cha Agano Jipya. Sura zake 16 zilizojaa vitendo vinafunua utambulisho wa kipekee, mafundisho na kazi ya Yesu. Injili inamaanisha 'habari njeri', na Marko anaelezea kitabu hiki kama “habari njema juu ya Yesu Masihi”.

Injili ni nini?

Biblia Takatifu inatufundisha kwamba watu wote wanastahili aibu na hukumu kwa dhambi zetu. Lakini habari njema ni kwamba Yesu alikufa msalabani na kuchukua hukumu tunayostahili. Alifufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu ili kuthibitisha kwamba amelipa dhambi ya kila mtu anayemwamini. Na tunapotumaini Yesu kama Bwana na Mwokozi, Mungu anatusamehe kikamilifu na milele. Tunapata uhusiano halisi na uliorejeshwa na Mungu ambao hautaishia kamwe.

Vidokezo vya kusoma

Unaweza kuvinjari kitabu hiki kwa nambari za sura na aya (angalia viungo chini ya ukurasa ili kubadilisha sura). Kwa mfano, 'Marko 8:29' inahusu Marko sura ya 8, aya ya 29. Kwa sababu Biblia ni kitabu cha zamani kutoka mahali pengine, kuna mambo mengi ambayo unaweza kuwa vigumu kuelewa mwanzoni. Hii inapotokea, ombe msaada wa Mungu, na fikiria kusoma kitabu na mfuasi mwenye uzoefu wa Yesu. Maoni ya mtandaoni kama vile bibleref.com pia yanaweza kukusaidia unapojifunza.

Marko

Marko 11

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake, 2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtampata mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. 3Mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”
4 Wakaenda, wakampata mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba. 5Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwana-punda?” 6Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu. 7Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda. 8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani. 9Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,
“Hosana!”
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”
10 “Umebarikiwa ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”
“Hosana kwake yeye aliye juu!”
11 Yesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
12 Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa. 13Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. 14Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.
15 Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, 16wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. 17Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa:
“ ‘Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote’?
Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’”
18 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote walishangazwa na mafundisho yake.
19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.
20 Kesho yake asubuhi walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. 21Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”
22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. 25Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”
27 Wakafika tena Yerusalemu, na Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wa watu wakamjia. 28Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”
29Yesu akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 30Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Niambieni!”
31Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ 32Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’ ” (waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yohana alikuwa nabii wa kweli); 33kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatujui.”
Naye Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

Unataka kwenda wapi baadaye?