Kuhusu injili ya Marko

Injili ya Marko ni rekodi ya kale iliyoandikwa zaidi ya Yesu wa Nazareti, iliyoandikwa karibu 65 BK na rafiki wa karibu wa Yesu na mwanafunzi wake, Petro. Marko ni sehemu ya Biblia Takatifu - kitabu cha pili cha Agano Jipya. Sura zake 16 zilizojaa vitendo vinafunua utambulisho wa kipekee, mafundisho na kazi ya Yesu. Injili inamaanisha 'habari njeri', na Marko anaelezea kitabu hiki kama “habari njema juu ya Yesu Masihi”.

Injili ni nini?

Biblia Takatifu inatufundisha kwamba watu wote wanastahili aibu na hukumu kwa dhambi zetu. Lakini habari njema ni kwamba Yesu alikufa msalabani na kuchukua hukumu tunayostahili. Alifufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu ili kuthibitisha kwamba amelipa dhambi ya kila mtu anayemwamini. Na tunapotumaini Yesu kama Bwana na Mwokozi, Mungu anatusamehe kikamilifu na milele. Tunapata uhusiano halisi na uliorejeshwa na Mungu ambao hautaishia kamwe.

Vidokezo vya kusoma

Unaweza kuvinjari kitabu hiki kwa nambari za sura na aya (angalia viungo chini ya ukurasa ili kubadilisha sura). Kwa mfano, 'Marko 8:29' inahusu Marko sura ya 8, aya ya 29. Kwa sababu Biblia ni kitabu cha zamani kutoka mahali pengine, kuna mambo mengi ambayo unaweza kuwa vigumu kuelewa mwanzoni. Hii inapotokea, ombe msaada wa Mungu, na fikiria kusoma kitabu na mfuasi mwenye uzoefu wa Yesu. Maoni ya mtandaoni kama vile bibleref.com pia yanaweza kukusaidia unapojifunza.

Marko

Marko 15

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza la Wayahudi lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Yesu, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.
2 Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu, “Wewe umesema.”
3Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi. 4Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”
5 Lakini Yesu hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa.
6 Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka. 7Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi. 8Umati ule wa watu wakamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.
9Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu mfalme wa Wayahudi?” 10Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mkononi mwake kwa ajili ya wivu. 11Lakini viongozi wa makuhani wakachochea umati ule wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.
12Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita mfalme wa Wayahudi?”
13Wakapiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
14Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakapiga kelele zaidi, wakisema, “Msulubishe!”
15 Pilato, akitaka kuridhisha umati ule wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Yesu apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
16 Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari. 17Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamvika kichwani. 18Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 19Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki. 20Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.
21 Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Iskanda na Rufo, alikuwa anaingia mjini kutoka mashambani, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 22Kisha wakampeleka Yesu hadi mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 23Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa. 24Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua.
25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. 26Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya:
Mfalme wa Wayahudi.
27 Pamoja naye walisulubiwa wanyangʼanyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [ 28Nalo andiko likatimizwa, lisemalo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.”] 29Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, 30basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!”
31 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa sheria wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32Basi huyu Kristo, huyu mfalme wa Israeli, ashuke sasa msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.
33 Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa. 34Hapo saa tisa, Yesu akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
35Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Eliya.”
36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”
37 Kisha Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.
38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini. 39Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Yesu aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
40 Palikuwa na wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwa Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome. 41Hawa walifuatana na Yesu na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwako wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye hadi Yerusalemu.
42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi (yaani siku moja kabla ya Sabato), 43Yusufu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na alikuwa anautarajia ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Yesu. 44Pilato alikuwa akijiuliza kama Yesu alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Yesu alikuwa amekwisha kufa. 45Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yusufu ruhusa ya kuuchukua huo mwili. 46Hivyo Yusufu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi. 47Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.

Unataka kwenda wapi baadaye?