Kuhusu injili ya Marko

Injili ya Marko ni rekodi ya kale iliyoandikwa zaidi ya Yesu wa Nazareti, iliyoandikwa karibu 65 BK na rafiki wa karibu wa Yesu na mwanafunzi wake, Petro. Marko ni sehemu ya Biblia Takatifu - kitabu cha pili cha Agano Jipya. Sura zake 16 zilizojaa vitendo vinafunua utambulisho wa kipekee, mafundisho na kazi ya Yesu. Injili inamaanisha 'habari njeri', na Marko anaelezea kitabu hiki kama “habari njema juu ya Yesu Masihi”.

Injili ni nini?

Biblia Takatifu inatufundisha kwamba watu wote wanastahili aibu na hukumu kwa dhambi zetu. Lakini habari njema ni kwamba Yesu alikufa msalabani na kuchukua hukumu tunayostahili. Alifufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu ili kuthibitisha kwamba amelipa dhambi ya kila mtu anayemwamini. Na tunapotumaini Yesu kama Bwana na Mwokozi, Mungu anatusamehe kikamilifu na milele. Tunapata uhusiano halisi na uliorejeshwa na Mungu ambao hautaishia kamwe.

Vidokezo vya kusoma

Unaweza kuvinjari kitabu hiki kwa nambari za sura na aya (angalia viungo chini ya ukurasa ili kubadilisha sura). Kwa mfano, 'Marko 8:29' inahusu Marko sura ya 8, aya ya 29. Kwa sababu Biblia ni kitabu cha zamani kutoka mahali pengine, kuna mambo mengi ambayo unaweza kuwa vigumu kuelewa mwanzoni. Hii inapotokea, ombe msaada wa Mungu, na fikiria kusoma kitabu na mfuasi mwenye uzoefu wa Yesu. Maoni ya mtandaoni kama vile bibleref.com pia yanaweza kukusaidia unapojifunza.

Marko

Marko 7

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
1 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu wakakusanyika mbele ya Yesu. 2Wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula kwa mikono iliyo najisi, yaani bila kunawa kama ilivyotakiwa na sheria ya dini ya Wayahudi. 3(Kwa kuwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali chakula pasipo kunawa kwa kufuata desturi za wazee wao. 4Wanapotoka sokoni hawawezi kula pasipo kunawa. Pia kuna desturi zingine nyingi wanazofuata kama vile jinsi ya kuosha vikombe, vyungu na vyombo vya shaba.)
5 Hivyo, wale Mafarisayo na walimu wa sheria wakamuuliza Yesu, “Mbona wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, na badala yake wanakula kwa mikono najisi?”
6 Yesu akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa:
“ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
7 Huniabudu bure,
nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’
8 Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.”
9 Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuyashika mapokeo yenu! 10Kwa mfano, Musa alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ 11Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia ni Korbani’ (yaani kimewekwa wakfu kwa Mungu), 12basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake. 13Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya aina hiyo.”
14 Yesu akaita tena umati ule wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, na mwelewe jambo hili. 15Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [ 16Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”
17 Baada ya Yesu kuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule. 18Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? 19Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni safi.)
20Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”
24 Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha. 25Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake. 26Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu.
27Yesu akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
28Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.”
29Ndipo Yesu akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.”
30Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.
31 Kisha Yesu akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli. 32Huko, watu wakamletea Yesu mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu.
33 Yesu akampeleka yule kiziwi kando, mbali na watu, akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34Ndipo Yesu akatazama mbinguni, akashusha pumzi kwa nguvu, akamwambia, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”) 35Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa.
36 Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowakanya, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii. 37Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”

Unataka kwenda wapi baadaye?